Katika Yuda 1:20, tunasoma jambo la kuvutia; inasema, “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu.” Neno “mkijijenga” kama lilivyotumiwa na Mtume Paulo halimaanishi kujenga kitu upya au kuanzia mwanzo; ni neno la Kiyunani “epoikodomeo.” Linamaanisha kujenga katika, au kujenga juu ya; yaani kujenga juu ya msingi uliokwishajengwa tayari.
Sasa, Biblia inatujulisha kuwa Mungu amemkirimia kila mtu kiasi cha imani (Warumi 12:3); kiasi cha imani ulichopewa na Mungu ndio msingi unaohitaji kujenga juu yake kwa ajili ya maisha ya ustawi, mafanikio, ushindi, afya ya Kiungu na utukufu kama atakavyo Mungu.
Mara kwa mara, kwa jinsi unavyokuwa unalisikia Neno la Mungu, imani inakuwa kubwa ndani yako, na unahamasika kuchukua hatua fulani. Huo ndio wasaa wako wa imani; huo ndio wakati ambao ni lazima uweke imani yako katika matendo. Endapo utachelewa, imani hiyo inaweza ikafifia au kusambaratika [kuyoyoma], kwa sababu imekuja katika Neno ulilolisikia wakati huo. Kile unachopaswa kufanya wakati imani imekuja kwako namna hiyo ni kuchukua hatua, na kisha kuendelea kuilisha imani yako na kuifanya kuwa imara [thabiti].
Mstari wetu mkuu unasema kuwa Mungu ndiye Anatenda kazi ndani yako kutaka kwako na kutenda kwako katika kulitimiza kusudi Lake jema. Muda wote huo uliokuwa umehamasishwa na kufikiri kufanya jambo kwa ajili ya Bwana au kuchukua hatua kwa ajili ya Injili, ilikuwa ni Mungu akiyatenda makusudi Yake ndani yako. Mara tu unapochukua hatua, usiiruhusu imani yako kushuka; jenga juu yake, kwa sababu kuna zaidi ya kutenda; dumisha imani yako kuwa hai. Hapa ndipo ambapo wengine hukosea; hawatambui ya kuwa wanapaswa kujenga imani yao katika hali endelevu; hivyo, wanajikuta wakiyumbayumba, na kusitasita juu ya Neno la Mungu kutokana na kutokuamini.
Pindi unapolisikia Neno la Mungu na imani ikaja kwako, tenda yaani weka imani yako katika matendo haraka sana; shikilia picha hiyo [maono hayo], na usiruhusu kitu chochote kukusimamisha. Yumkini ni mafundisho kuhusiana na kutoa, na imani yako imehamasishwa [imechochewa] kutoa, songa mbele na fanya hivyo haraka; kamatia wasaa huo wa imani na litende Neno.
Kamwe usikae uruhusu hamasa ya imani yako kufifia; dumisha imani yako kuwa moto-moto; jenga na inawirishe kwa Neno la Mungu na usiruhusu nafasi kwa ajili ya maneno hasi ambayo yanazaa mashaka, na kuchelewesha baraka za kulitenda Neno.
