Ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu (Wakolosai 1:27).
Wengi wanafikiri kuwa Ukristo uliturudisha katika kile ambacho Adamu na Hawa walikuwa au walichokuwa nacho katika Bustani ya Edeni, lakini hilo si kweli. Kile tulichonacho ni utukufu mkuu zaidi (2 Wakorintho 3:10). Kwa kuzaliwa mara ya pili, haujazaliwa kutokana na Adamu wa kwanza bali umezaliwa kutokana na Adamu wa pili na wa mwisho, Yesu Kristo. Maandiko yanasema, “Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi hai. Bali Adamu wa mwisho—ambaye ni, Kristo—ni roho yenye kuhuisha”
(1 Wakorintho 15:45 Biblia toleo la NLT).
Ninataka uangalie kwa makini njeo [wakati] uliotumika katika Warumi 8:30 kwa tunavyosoma kutoka katika Agano Jipya la Biblia ya toleo la Weymounth: “na wale Yeye aliowachagua tangu asili pia Aliwaita; na wale ambao Yeye aliwaita pia Alitangaza kuwa hawana hatia; na wale ambao Yeye alitamka kuwa hawana hatia hao pia Aliwavika taji ya utukufu.” Hapa, tunaona vitambulishi vya muhimu kuhusiana na kiumbe kipya, tu matunda yaani matokeo ya kazi ya ukombozi ya Kristo; ambapo mojawapo ni kuwa umevikwa utukufu. Hii ina maana kwamba umeletwa katika maisha ya uzuri na ubora.
Zaidi sana, katika 1 Petro 5:10 tunasoma kuwa Mungu amekuita katika utukufu Wake wa milele katika Kristo Yesu. Kweli kama hiyo pia imesisitizwa katika 2 Petro 1:3 (Biblia toleo la KJV): “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita katika utukufu na ubora.” Umetukuzwa; sio kwa utukufu wowote mdogo, bali kwa utukufu ule ule ambao u juu ya Yesu. Alisema katika Yohana 17:22: “Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao…”
“Lakini je! Biblia haisemi katika Warumi 3:23 kuwa wote tumetenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu?” Mtu anaweza akahoji. Unapaswa kujua hilo lilikuwa ni kabla ya Yesu kuja. Watu wote walitengwa mbali na utukufu wa Mungu kwa sababu ya dhambi, lakini Yesu, kupitia kifo Chake, alizigongomelea dhambi pale msalabani na kutuleta katika utukufu; na sio katika utukufu ambao Adamu na Hawa walikuwa nao, bali katika utukufu wake Mwenyewe; Alikutukuza wewe kwa Yeye mwenyewe.
Ikimzungumzia Yesu, Waebrania 2:9 inatujulisha kwamba Mungu amemvika taji ya utukufu na heshima. Kisha katika 1 Yohana 4:17 tunasoma kuwa na kama Yeye alivyo, ndivyo tulivyo ulimwenguni humu. Atukuzwe Mungu! Umevikwa taji ya utukufu na heshima kama Yesu. Maisha yako si kwa ajili ya fedheha [aibu]; bali kwa ajili ya utukufu, uzuri, ubora na heshima. Haleluya!
